Kiswahili na Uchumi wa Kidijitali
Synopsis
Chapisho hili lenye anwani Kiswahili na Uchumi wa Kidijitali ni zao la makala teule zilizofanyiwa utafiti wa kina na kuwasilishwa katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro mnamo Machi 2024. Kongamano hilo liliwaleta pamoja wataalam na wakereketwa wanaohusika na malezi ya lugha adhimu ya Kiswahili kutoka vyuo vikuu na taasisi nyinginezo ulimwenguni. Kongamano hilo lilitoa fursa nzuri kwa wataalam kujadili upekee na uwezo wa lugha ya Kiswahili wa kutumiwa katika kuendeleza uchumi wa kidigitali. Aidha, mabingwa hawa walikongamana ili kudhihirisha namna ambavyo Kiswahili kinatumiwa katika majukwaa mbalimbali ya kidijitali, hivyo kukikuza na kukiwezesha kuwa lugha ya matumizi mapana ulimwenguni. Chapisho hili limegawika katika sura nne ambapo masuala anuwai yanayohusu maendeleo ya elimu, lugha, isimu na fasihi ya Kiswahili katika ulimwengu wa kidijitali yamepambanuliwa kwa utondoti. Mathalani, Sura ya Kwanza imeshughulikia masuala ya Fasihi Andishi katika Enzi ya Kidijitali, huku Sura ya Pili ikiangazia taaluma ya Fasihi Simulizi katika Enzi ya Kidijitali. Kadhalika, Sura ya Tatu imedadavua masuala ya Elimu ya Kiswahili katika Enzi ya Kidijitali. Hatimaye, Sura ya Nne imepambanua namna ambavyo Kiswahili kinatumiwa katika Ujasiriamali, Ubidhaaishaji na Uchumi wa Kidijitali. Kitabu hiki basi kitakuwa hazina aali kwa wasomi na watafiti wa taaluma za Kiswahili.
Published
License

This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.
